Tanzania ni jamhuri ya muungano iliyoundwa baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964. Lakini ni taifa lenye historia ndefu. Haya hapa matukio makuu historia ya taifa hilo.
1498 - Mreno Vasco da Gama afika pwani ya Tanzania.
1506 – Wareno wafanikiwa kudhibiti maeneo karibu yote ya pwani ya Afrika Mashariki.
1699 – Wareno wafurushwa kutoka Zanzibar na Waarabu kutoka Oman.
1884 – Shirika la German Colonisation Society lililoanzishwa na Mjerumani Carl Peters laanza kuchukua umiliki wa maeneo Tanzania bara.
1886 – Uingereza na Ujerumani zatia saini mkataba wa kuruhusu Ujerumani kudhibiti maeneo ya Tanzania bara ila tu ukanda mwembamba maeneo ya pwani ambao unasalia chini ya sultani wa Zanzibar. Zanzibar yaendelea kuwa nchi lindwa ya Uingereza.
1905-06 – Wapiganaji wa Maji Maji washindwa na wanajeshi wa Ujerumani.
Kutawaliwa na Uingereza
1916 – Wanajeshi wa Uingereza, Ubelgiji na Afrika Kusini washinda wanajeshi wa Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kukalia Afrika Mashariki ya Kijerumani. (Eneo la Afrika Mashariki ya Kijerumani lilijumuisha Tanganyika na Rwanda na Burundi).
1919 – Muungano wa Mataifa waiteua Uingereza kuwa mdhamini wa Tanganyika – ambayo sasa ndiyo Tanzania bara.
1929 – Chama cha Tanganyika African Association (TAA) chaanzishwa.
1946 – Umoja wa Mataifa wabadilisha idhini ya Uingereza Tanganyika kutoka kwa mdhamini hadi kuwa mlezi.
1954 - Julius Nyerere na Oscar Kambona wabadilisha chama cha Tanganyika African Association kuwa Tanganyika African National Union (TANU).
Uhuru
1961 - Tanganyika yajipatia uhuru Julius Nyerere akiwa waziri mkuu.
1962 - Tanganyika yawa jamhuri Nyerere akiwa rais.
1963 - Zanzibar yajipatia uhuru wake.
1964 – Sultani wa Zanzibar apinduliwa na chama cha Afro-Shirazi Party kwenye mapinduzi ya mlengo wa kushoto yaliyokuwa na ghasia; Tanganyika na Zanzibar zaungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nyerere akiwa rais wa jamhuri hiyo mpya na kiongozi wa serikali ya Zanzibar na kiongozi wa chama cha Afro-Shirazi Party, Abeid Amani Karume, akiwa makamu wa rais.
1967 - Nyerere atoa Azimio la Arusha, ambalo linahimiza usawa, ujamaa na kujitegemea.
1974: Serikali yatangaza kuhamisha mji mkuu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Mji wa Dar es Salaam ulikuwa mji mkuu chini ya Wajerumani kuanzia 1891 hadi 1916 na pia kuanzia 1964.
1977 – Chama cha Tanganyika
African National Union (TANU) na chama cha Afro-Shirazi Party cha Zanzibar vyaungana na kuwa Chama cha Mapinduzi, ambacho kinatangazwa kuwa chama pekee kinachotambuliwa kisheria.
1978 – Uganda chini ya Idi Amin yavamia na kudhibiti kwa muda maeneo ya ardhi ya Tanzania.
1979 – Vikosi vya Tanzania vyavamia Uganda, vyadhibiti mji mkuu Kampala, na kusaidia kumuondoa madarakani Rais Idi Amin.
Siasa za vyama vingi
1985 - Nyerere astaafu na nafasi yake kuchukuliwa na rais wa Zanzibar, Ali Mwinyi.
1992 – Katiba yafanyiwa marekebisho kutoa nafasi kwa siasa za vyama vingi.
1995 - Benjamin Mkapa achaguliwa kuwa rais wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi.
Shambulio ubalozi wa Marekani
1998 Agosti 7 – Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania walipuliwa kwa bomu. Shambulio sawa latekelezwa ubalozi wa Marekani taifa jirani la Kenya.
1999 Oktoba 14 – Mwanzilishi wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki.
2000 - Mkapa achaguliwa kuongoza kwa muhula wa pili, akipata 72% ya kura.
2001 26 Januari – Polisi wa Tanzania waua kwa kupiga risasi watu wawili Zanzibar wakishambulia afisi za chama cha Civic United Front (CUF) mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba ashtakiwa kuandaa mkutano haramu na kuvuruga amani.
Machafuko Zanzibar
2001 27-28 January - Watu 31 wauawa na wengine 100 kukamatwa Zanzibar kwenye maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya kupiga marufuku mikutano ya upinzani ya kuitisha uchaguzi mpya. Serikali ya Tanzania yatuma wanajeshi kudhibiti hali.
2001 Machi – Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na chama kikuu cha upinzani Zanzibar, CUF, vyakubaliana kuunda kamati ya pamoja kurejesha utulivu na kuhimiza watu waliotorokea Kenya kurejea.
2001 Aprili – Maelfu ya wafuasi wa vyama vya upinzani waandamana katika mji wa Dar es Salaam, kwenye maandamano ya kwanza makubwa kufanywa na upinzani katika miongo kadha.
2001 Julai – Mgodi mkubwa wa dhahabu, Bulyanhulu, wafunguliwa karibu na mji wa Mwanza kaskazini mwa Tanzania, na kufanya Tanzania kuwa mzalishaji wa tatu wa dhahabu kwa ukubwa Afrika.
2001 Novemba – Marais wa Tanzania, Uganda na Kenya wazindua bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mahakama mjini Arusha kushughulikia masuala ya pamoja kama vile biashara na uhamiaji.
2001 Desemba – Uingereza yaidhinisha mkataba wenye utata wa kuuzia Tanzania mfumo wa jeshi wa kudhibiti safari za ndege. Wakosoaji wasema huko ni kutumia pesa vibaya.
2002 Juni – Takriban watu 300 wauawa katika mkasa mbaya zaidi wa treni Tanzania baada ya gari moshi la kubeba abiria kugongana na gari moshi la kubeba mizigo.
2002 Agosti – Upinzani wamshutumu rais kwa kununua ndege ya kumbeba ya $21m (£14m).
2005 Machi-Aprili – Machafuko ya kisiasa yashuhudiwa Zanzibar kabla ya usajili wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba.
2005 Oktoba – Chama tawala CCM chashinda uchaguzi Zanzibar. Upinzani CUF wadai kumekuwa na wizi wa kura na kutangaza kususia shughuli za bunge Zanzibar.
Kikwete achaguliwa
2005 Desemba - Jakaya Kikwete, aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni na mgombea wa CCM, ashinda uchaguzi wa urais. Amrithi Benjamin Mkapa, aliyestaafu baada ya kuongoza mwongo mmoja.
2006 Aprili – Mahakama Kuu yaharamisha utamaduni wa kutumbuiza wagombea nyakati za uchaguzi. Wakosoaji wa desturi hiyo ya "Takrima" – kutoa zawadi – wasema ilichangia rushwa.
2006 Juni – Waziri Mkuu wa Uchina Wen Jiabao, aliyezuru Tanzania ikizwa nchi yake ya saba kutembelea kwenye ziara yake barani, atia saini mikataba ya kawi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, na kutia saini mikataba ya kusaidia sekta za afya, uchukuzi na mawasiliano Tanzania.
2006 Agosti – Benki ya Maendeleo ya Afrika yatangaza kufutiliwa mbali kwa deni la zaidi ya $640m ambalo Tanzania ilidaiwa. Benki hiyo yasema imefurahishwa na rekodi ya uchumi wa Tanzania na viwango vya uwajibikaji kuhusu fedha za umma.
2007 Januari – Maafisa wa Afisi ya Uingereza ya kufuatilia makosa ya Ulaghai wafika Tanzania kuchunguza ununuzi wa mfumo wa jeshi wa kudhibiti safari za ndege wa 2001. Gazeti moja la Uingereza laripoti kuwa kampuni ya BAE Systems, ililipa $12m kwa Mtanzania mmoja ili kushinda zabuni hiyo.
2007 Julai – Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton azindua mpango wenye lengo la kuwezesha kupatikana kwa dawa za malaria kwa bei nafuu. Mpango huo wa majaribio ulikuwa baadaye upanuliwe hadi maeneo mengine Afrika.
2008 Januari – Gavana wa Benki Kuu Daudi Ballali afutwa baada ya ukaguzi wa hesabu wa kimataifa kuonyesha benki hiyo ilifanya malipo yasiyofaa ya zaidi ya $120m (£60m) kwa kampuni za Tanzania.
Kashfa
2008 Februari – Rais avunja baraza lake la mawaziri kufuatia kashfa ya ulaji rushwa ya Richmond iliyomfanya waziri wake mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu. Bw Lowassa amekana kuhusika katika kashfa hiyo.
2009 Novemba – Chama cha upinzani Zanzibar, CUF, chasitisha mgomo wake wa kususia shughuli za bunge la visiwani huku uchaguzi mkuu ukikaribia.
2010 Julai - Tanzania yaungana na jirani zake kuunda soko la pamoja la Afrika Mashariki kwa lengo la kutangamanisha chumi za mataifa ya eneo hilo.
2010 Septemba - Rais Kikwete asema ujenzi wa barabara ya kupitia mbuga ya wanyama pori ya Serengeti utaendelea, licha ya mradi huo kupingwa na wataalamu wa mazingira.
2010 Oktoba – Rais Kikwete achaguliwa kuongoza muhula wa pili.
2010 Desemba – Kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza silaha Uingereza, BAE Systems, yapigwa faini kuhusiana na zabuni ya kuuzia Tanzania mfumo wa rada. Zabuni hiyo ilijaa utata.
2011 Januari – Watu wawili wauawa polisi wakitawanya waandamanaji waliokuwa wakiitisha kuachiliwa huru kwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema Freeman Mbowe, aliyezuiliwa kabla ya mkutano wa kisiasa wa upinzani wa kulalamikia ufisadi serikalini.
2011 Julai – Kampuni ya Uingereza BAE Systems yakiri kulipa £8m ili kupata zabuni ya kuuzia Tanzania mfumo wa usimamizi wa safari za ndege mwaka 1999, yakubali kulipa Tanzania fidia ya £30m.
2012 Machi – Kampuni za kupeleleza mafuta za Statoil na Exxon Mobil zagundua kuwepo kwa gesi nyingi zaidi katika pwani ya Tanzania. Eneo hilo lenye gesi la Zafarani limo karibu na eneo la pwani ya Msumbiji ambako gesi nyingine nyingi inachimbwa na kampuni za Anadarko na ENI.
2012 Mei – Rais Jakaya Kikwete awafuta kazi mawaziri sita baada ya mkaguzi wa fedha za umma kugundua “ubadhirifu mkubwa wa fedha” katika wizara saba. Mawaziri wa fedha, kawi, utalii, biashara, uchukuzi na afya wapoteza kazi.
2012 Agosti - Tanzania yathibitisha meli 36 za kubeba mafuta za Iran zimekuwa zikitumia bendera ya Tanzania kukwepa vikwazo vya Marekani na Muungano wa Ulaya vya kuizuia kuuza nje mafuta yake. Marekani yaonya Tanzania huenda ikawekewa vikwazo hilo lisipokoma.
2012 Oktoba – Polisi wakamata watu 126 kuhusiana na kushambuliwa kwa makanisa matano Dar es Salaam. Waislamu waliharibu na kuchoma makanisa hayo baada ya mvulana Mkristo kudaiwa kukojolea nakala ya Koran.
2013 Machi – Rais mpya wa Uchina Xi Jinping atembelea Tanzania kwenye sehemu ya ziara yake Afrika. Aliandamana na mkewe Peng Liyuan.
2013 Mei – Shambulio la bomu katika kanisa mpya la Kikatoliki mjini Arusha laua watu wawili na kujeruhi wengine kadha.
2013 Julai – Rais wa Marekani Obama na rais wa zamani wa Marekani George W Bush waweka shada la maua kwenye hafla ya kuwakumbuka wahasiriwa na waathiriwa wa shambulio la bomu ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.
2013 Agosti – Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lasema maelfu ya watoto hufanya kazi katima machimbo madogo ya dhahabu Tanzania, jambo linalohatarisha afya yao.
2013 Novemba – Maafisa wa serikali wanasa zaidi ya pembe miama saba zikiwa zimefichwa katika nyumba ya raia wa Uchina jijini Dar es Salaam.
2013 Desemba – Mawaziri wane wafutwa kazi kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za kibinadamu wakati wa kukabiliana na uwindaji haramu wa wanyamapori.
2014 Aprili - Tanzania yaadhimisha miaka 50 ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.
2014 Mei – Waganga wawili wakienyeji wakamatwa baada ya kuuawa kwa albino.
2014 Julai – Watu wanane wajeruhiwa katika mlipuko wa bomu hoteli maarufu ya watalii Arusha.
2014 Oktoba – Watu saba waliodaiwa kuwa wachawi wachomwa wakiwa hai eneo la magharibi la Kigoma. Kundi moja la huko lasema watu 500 huuawa kila mwaka wakishukiwa kuwa wachawi.
2015 Januari – Serikali yapiga marufuku waganga wa kienyeji, lengo likiwa kukomesha visa vya kushambuliwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino.
2015 Aprili – Kura ya maamuzi kuhusu katiba mpya yaahirishwa baada ya kucheleweshwa kwa usajili wa wapiga kura.
2015 Oktoba - Dkt John Pombe Magufuli wa CCM atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 25.
No comments:
Post a Comment