RAIS John Magufuli alipoingia katika Ikulu ya Magogoni miaka mitatu iliyopita, watalaam wa masuala ya Siasa na uchumi hawakutaraji kuyaona mafanikio makubwa ya kiuchumi ndani ya muda mfupi kama inavyotokea sasa.
Kinachotokea sasa hivi ni kama muujiza, kwani mamia ya matrilioni ya fedha za kuendesha miradi ambayo tayari imeanzishwa na Serikali hayakuonekana wala hayakujulikana yangepatikanaje kuihudumia miradi hii mikubwa katika historia ya uchumi wa taifa letu.
Walioamini hivyo, hawawezi kuhukumiwa kwamba walikuwa ni wajinga, mbumbu wala majuha katika masuala ya uchumi bali waliongozwa na mifumo ya uchumi iliyokuwa legelege ambayo kwa bahati mbaya wakati huo, ndio ilikuwa inaonekana bayana machoni pao na pia ndani ya makabrasha ya Serikali.
Kama si kasi ya utekelezwaji wa ahadi na miradi hiyo, inayotekelezwa sasa na Serikali yake, tena ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu ya kuwepo kwake madarakani, bado wangeendelea kuamini hata leo kwamba malengo haya hayawezekani, mipango hii haiwezekani, fikira hizi ni za kufikirika, kama si kusadikika na kadhalika!
Lakini sasa, katika miaka mitatu ya uongozi wake, JPM amefanikiwa pengine kwa asilimia zaidi ya asilimia 100 kwani kwa vipindi fulani, mamlaka zilizokuwa madarakani hazikuweza kutimiza hata asilimia 50 ya aliyoyafanya Rais Magufuli hata ndani ya kipindi cha miaka kumi zaidi ya kujenga matumaini na matarajio ya mambo yatakayofanyika baada ya muhula wa uongozi wao kumalizika.
Katika utekelezaji wa azma yake hiyo, kuna miradi au fikira za miradi hiyo, iliyoonekana kama ni uendawazimu kuifikiria hata kabla ya kueleza uwezekano wa kutekelezwa kwake.
Baada ya kuingia madarakani, Magufuli hakuanza taratibu utekelezwaji wa ahadi za ujenzi wa uchumi tena kupitia miradi mikubwa kama ilivyozoeleka kwa marais wengi wanaokamata madaraka.
Marais au viongozi wakuu wa nchi wanapokamata madaraka kwa desturi huanza taratibu utekelezaji wa shughuli za kiuongozi na maamuzi kwa kisingizio cha kuyazoea madaraka na hofu ya kukosea au kuwaudhi watu ambao kwa siri au bayana huaminika wana siri kubwa katika Ikulu na maeneo mbalimbali muhimu na nyeti katika serikali na taasisi zake.
Hofu hii hutokana na mazingaombwe yanayoitwa kukosa uzoefu na kuhofia hujuma zinazoweza kufanywa na wakubwa wenzie, wanaoongoza taasisi nyeti zenye kuhifadhi nyaraka muhimu na wanaodhibiti nyendo muhimu za kiuongozi na kiuelekezaji huku wakiwa na ushawishi mkubwa juu ya wale wanaowaongoza na hivyo kukorofisha kwao wanaamini kwamba kunaweza kuzalisha uasi unaoweza ama kuidhoofisha serikali yake au kuiondosha kabisa madarakani.
Hofu hii ya kuhujumiwa , mara nyingi hukisiwa kufanywa na wapambe wa kiongozi mkuu wanaokuwa naye mara kwa mara wakijifanya ndio masikio yake, macho yake na hata wakati mwingine kwamba ni fikira zake( yaani wanaofikiri kwa niaba ya kiongozi).
Matokeo ya uwepo wa fikira hizi na watu hawa huwasababisha viongozi wengi kuwa na hofu ya kuyatekeleza kwa ufasaha yale yaliyokuwa ndani ya vichwa vyao kabla ya kuingia madarakani, hapa ikumbukwe kuwa kabla ya kuwa kiongozi mkuu, mtu huwa huru kwani huwa kuna taratibu chache zinazombana kutekeleza yale anayoyatamani kuyaona yakifanyika kwa wakati muafaka.
Baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi, kuna Mkurulo wa itifaki zinazotakiwa kutekelezwa na kiongozi huyo, kwa mfano, ni wakati gani wa kula, chakula kipikwe na nani, nani akitie mezani, nani akionje, alale wapi, saa ngapi, aseme nini, kwa njia gani, aende wapi, lini, na kwa njia gani? Haya ni miongoni mwa taratibu nyingi zinazotakiwa kutekelezwa na kiongozi mkuu wa nchi.
Ni vigumu kuamini basi, kwamba JPM na maamuzi anayoyafanya yanatokana pengine na kubadilika kwa taratibu za kitaasisi katika Ikulu ya Magogoni? Pengine ukali wake na kutokukubali mambo kufanyika kutokana na matakwa ya taratibu tu na badala yake mazingira na matakwa ya wakati kuamua ni jambo gani lifanyike na kwa jinsi gani ndiyo nyenzo inayomsaidia kutekeleza maamuzi yanayohusu mustakabali wa taifa hili kiuchumi?
Mjadala ni mrefu kila jambo linaweza kuwa sahihi kutokana na wakati ule linapojadiliwa lakini kimsingi, JPM amefanikiwa vikubwa kubadili mwelekeo na utamaduni wa utekelezaji wa maamuzi au matakwa ya uchumi kutokana na dhamira yake, ujasiri, uzalendo na pia matakwa ya kuliona taifa likipiga hatua aliyoiikusudia kwa niaba ya Watanzania na kuacha itifaki ifanye kazi katika mfumo chanya.
UTEKELEZAJI WA MIRADI
MIRADI YA KIUCHUMI
Katika hali isiyofahamika vizuri, Serikali chini ya JPM, imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa na mingi kwa wakati mmoja na ndani ya muda mfupi kwa kipindi cha miaka mitatu. Miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa inayogharimu takribani trilioni sita za fedha za kitanzania, inatajwa kuwa gharama halisi ya mradi wa SGR. Iwapo gharama hazitaongezeka kutokana na thamani ya Dola dhidi ya shilingi.
Ujenzi wa reli hii ambayo itakuwa na vituo maalum vya kusimama kupakua na kupakia abiria na mizigo katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Kigoma, na Tabora na Mwanza inayojengwa kwa urefu wa km 726 na kutoa ajira 30,000 itakapokamilika ina manufaa makubwa kwani uanzishwaji wa miji katika maeneo haya ya vituo ni jambo lisilokwepeka.
SGR kwa sasa inajengwa kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi ni kutoka Dar es Salaam-Morogoro (Km 300) kwa gharama ya sh trilioni 2.8, awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora –Dodoma (km 400) kwa gharama ya Sh trilioni 4.3 ambapo uzinduzi wake ulianza rasmi Machi mwaka 2018.
Miji hii midogo inaweza kukua na kuwa miji mikubwa kutokana na uwepo wa vituo hivi vya treni ikizingatiwa kuwa mahitaji ya kiuchumi na kibinadamu yatakuwa ni kipaumbele. Maduka ya jumla na rejareja yatalazimika kujengwa na wafanyabiashara ili kukidhi matakwa na mahitaji ya kibiashara na kihuduma kwenye maeneo ya karibu na mbali kutoka eneo la kituo.
Vituo vya afya bila shaka vitajengwa kwenye maeneo hayo, ili kutoa huduma ya afya kwa wakazi wa miji hiyo midogo itakayoanza kukua ama taratibu ama kwa kasi kutokana na hali ya biashara itakavyokuwa kwa wakati huo. Miundombinu ya huduma kama nyumba za kulala wageni mbali ya nyumba za wenyeji, vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wa watu na mali zao.
Maeneo mengine ni pamoja na nyumba za maaskari na familia zao zitalazimika kujengwa na hivyo kuongeza ukubwa na ukuaji wa miji, shule za msingi na sekondari kwa ajili ya wafanyakazi na wakaazi na shughuli nyingine za kibinadamu zitajengwa na kuyafanya maeneo haya kuwa vituo vya kibiashara.
Utekelezwaji wa mradi huu, unaogharimu fedha nyingi tayari ulikuwa umepingwa na wafadhili wengi na hata mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kwa visingizio vya uharibifu wa mazingira, kutishia wanyama katika maeneo mbalimbali ya nchi, kuharibu ikolojia. Lakini kwa ujasiri wa JPM alipuzilia mbali maonyo yenye vitisho ya kuzuia uthubutu na mafanikio, yaliyolengwa kwa kuwepo na mradi huu.
Akitilia maanani siasa za Ulaya juu ya uchumi wa Afrika, kama yalivyo mawazo ya wasomi wenye uzalendo wa kiafrika kama alivyokuwa Profesa Walter Rodney katika kitabu chake cha “ How Europe Underdeveloped Africa”, yaani kwa tafasiri isiyo rasmi Jinsi Ulaya ilivyorositisha uchumi wa Afrika hii ni tafsiri yangu.
JPM akaamua kutia pamba masikioni na kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi bila kujali kelele za wazungu kwa kutilia maanani kwamba wazungu wanatamani kuendelea kuifanya Afrika kuwa shamba la bibi huku wakiendelea kutuimbia kwamba Afrika ni Bara la giza, maskini, maradhi na wakazi wake ni watu wasio sitaraabika.
Mradi wa Stigler (Bonde la Mto Rufiji) ni mawazo ya Hayati Mwl Julius Nyerere mara baada ya taifa hili kujipatia uhuru. Nia ya Mwalimu ilikuwa ni kulifanya taifa letu kujitosheleza na nishati ya umeme kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kuwekwa kwa jiwe la msingi kwa mradi huu uliofanywa hivi karibuni na JPM, ni kuifufua nia ya kishujaa ya Mwl Nyerere na kuyashinda majaribu na nia ovu ya mataifa ya Ulaya na Marekani ya kuzuia uwezekano wa Afrika kujitegemea kiuchumi na kuondokana na kasumba ya umaskini kwa watu wake iliyoenezwa kwa jitihada kubwa na kwa gharama na wakoloni wa kizungu na vibaraka wao walioitawala Afrika kwa wakati ule na mifumo ya ukoloni mamboleo inayoitawala Afrika kwa sasa. Imezoeleka miradi mikubwa kutekelezwa tu katika nchi za Ulaya na kwa siku za karibuni, katika nchi za Asia.
Sasa historia imebadilika, na inabadilika kwa kasi, kwani ujenzi wa miradi mikubwa unasikika kila mahali katika Jamhuri yetu ndani ya miaka mitatu pekee miradi mikubwa mitano inayogharimu matrilioni ya fedha za kitanzania imezinduliwa rasmi.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Ziwa Albert (Hoima) nchini Uganda hadi Tanga ambao unatarajia kugharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 3.55, ambao ujenzi wake unapitia katika wilaya 24 na jumla ya vijiji 184 katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Miradi mingine iliyopata mafanikio katika kipindi hiki cha miaka mitatu ni ya ujenzi wa miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege, viwanda vya madawa, ununuzi wa ndege kubwa kubwa.
Juhudi za sasa za Serikali ya awamu ya tano zimezalisha dhamira madhubuti sio ya kulihuisha tu Shirika letu la ndege bali kulipa sura mpya, ufanisi mpya wa kiutendaji na kiuongozi kwa kuagiza ndege mpya za kisasa zipatazo saba hadi sasa zikiwemo ndege zenye kunywa mafuta kidogo mno na kutua katika viwanja vya kila aina, aina yaBombardier Q400, Dream liner ya kisasa Boeing 787-8, Air bus A 220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 130ikiwa ni moja ya ndege mbili za aina hiyo zinazotarajiwa kuwasili nchini sanjari na uzinduzi wa miradi mikubwa ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo mradi mkubwa wa maji wa Nyamazugo ulioko wilayani Sengerema-Mwanza, Arusha, Ruvu-Pwani, Uvinza-Kigoma kwa kutaja michache.
SEKTA AFYA
Kwa upande wa Sekta ya afya, utekelezaji wa agizo la Rais kujenga vituo vya afya kila kata na baadaye kila kijiji umezinduliwa na tayari unaendelea ambapo jumla ya vituo vya afya 117 na vituo vingine 170 vimejengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 160, ambapo vituo hivyo kwa sasa vina uwezo wa kufanya upasuaji na huduma ya mama na mtoto haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia kama taifa.
Aidha serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 270 kwa mwaka 2018. imeongezeka ambayo ni sawa na zaidi ya asilimia 200. Mafanikio mengine katika kipindi hiki cha miaka mitatu ni kuwepo kwa huduma za upasuaji wa moyo na upandikizwaji wa viungo kama figo na vinginevyo unafanyika sasa nchini katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Mloganzila huku hospitali ya Bugando jijini Mwanza ikijimaarisha kwa kasi katika huduma hiyo muhimu nay a hatari.
Hatua hii ya upandikizaji wa viungo na matibabu ya moyo umeokoa mabilioni ya fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kuwapeleka watu kutibiwa nje ya nchi katika hosipitali za Apollo huko India, Afrika Kusini, Ujerumani, Israel, Uingereza na Marekani.
ELIMU
Kwa upande wa sekta ya elimu, ongezeko la fedha za serikali kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi limeleta ahueni kubwa kwa wazazi pamoja na kuwepo kwa changamoto kwa kada ya ualimu, ambapo bajeti ya fedha za mikopo kwa wanafunzi imeboreshwa zaidi.
Mfano idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo kwa sasa imeongezeka kutoka wanafunzi 98,000 waliokuwa wanapata mkopo kabla JPM hajaingia madarakani ambapo walikuwa wanapata mkopo wa Sh bilioni 340 tu, lakini katika mwaka 2016/17 wanafunzi 120,000 walifanikiwa kupata mkopo wa sh bilioni 483, ambapo kwa mwaka 2018/19 jumla ya wanafunzi 40,000 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 7000 wanatarajia kupata mkopo wa Sh bilioni 437! Lakini pia kwa mwaka 2017/18 wanafunzi 33,000 walinufaika na mkopo wa Sh biliioni 427, hivyo utaona kazi kubwa inayofanywa na serikali ya kuongeza idadi ya fedha za mkopo mwaka hadi mwaka!
Kuhusu masuala ya upandishaji madaraja na marupurupu mengine, ongezeko la madarasa, ongezeko la nyumba za walimu na kutegua kitendawili cha madawati na meza za kusomea lakini pia kuongezeka kwa fedha za serikali zinazoingia katika uendeshaji wa elimu ya msingi, kuboresha msingi wa vitabu vya ziada na kiada na hata kuviondoa baadhi ya vitabu vinavyosababisha mkanganyiko wa ufundishaji na kutatiza mtaala wa elimu kwa kiasi kikubwa kunaonyesha nia ya serikali ya kushughulikia kwa kasi matatizo katika elimu ya msingi, sekondari na vyuo.
Aidha upande wa elimu bila malipo imeendelea kuboreshwa, ambapo idadi ya wanafunzi, tangu mpango huo uanzishwe imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,000 mwaka 2015 hadi wanafunzi 1,896,000 mwaka 2016 kwa shule za msingi nchini na hivyo kufanya wanafunzi kutoka kaya ambazo hazina uwezo wa kuwasomesha kupata fursa hiyo ya adimu ya kuwapeleka shuleni.
MIUNDOMBINU
Kuimarishwa na kuanzishwa kwa miundombinu mipya ya barabara kunalisaidia taifa letu kumaliza mkwamo wa kiuchumi katika eneo hili, katika kushughulikia jambo hili tumeziona juhudi za mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kujenga barabara za juu kwa juu (Fly overs) kama daraja la Mfugale, Ubungo na upanuzi wa njia nane wa barabara ya Kimara hadi Kibaha jijini Dar es Salaam.
Miundombinu mingine ni pamoja na ujenzi wa daraja la Surrender unaoambatana na njia ya mkato kutoka hosipital ya Ocean Road hadi Kenyata Drive kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam, ujenzi wa daraja la juu ya ziwa Victoria la Kigongo-Busisi ambao usanifu wake unaendelea ni miongoni mwa miradi ya serikali inayoendelea kuonyesha nia yake kwamba sio nguvu ya soda bali ni dhamira yenye malengo ya kulifanya taifa letu kuwa la kisasa katika Afrika.
Orodha ni ndefu ya mambo mengi aliyotekeleza Mheshimiwa Rais, hivyo ni wakati mwafaka kwa raia wote wa Tanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa, kumuunga mkono katika kutimiza kwa pamoja malengo ya kuishi maisha bora na sio kumfanya Mheshimiwa Rais kujiona yuko peke yake kwenye njia hii ngumu ya kuleta maendeleo endelevu na mapinduzi ya kiuchumi katika taifa letu. Mungu ibariki Tanzania, tukutane kazini!
No comments:
Post a Comment